Mkemia Mkuu wa Serikali, Profesa Samuel Manyele
alitoa maelezo hayo alipoulizwa na gazeti hili kama ofisi yake inajua
madhara ya zebaki na sababu za kushindwa kudhibiti kusambaa kwa kemikali
hiyo iliyopigwa marufuku kimataifa. Madini hayo yanatumika kwenye
machimbo madogo katika maeneo mbalimbali nchini.
Profesa Manyele alisema madhara ya zebaki ni
pamoja na kansa na magonjwa ya ngozi na yapo mengine ambayo hayajitokezi
mapema, lakini ni mabaya zaidi kwa vile uharibu maeneo muhimu ya mwili
kama kupooza uti wa mgongo na kuharibu maumbile ya mbegu za uzazi.
Akizungumzia ugumu wa kuzuia kemikali hiyo,
Profesa Manyele alisema ni sawa na ile ya dawa za kulevya na kibaya
zaidi ni kuona halmashauri nchini zinachukua ushuru kwa watu wanaotumia
kemikali hizo na pia Wizara ya Nishati na Madini nayo inatoa vitalu kwa
watu wanaotumia kemikali hiyo.
“Kinachotakiwa sasa ni kwa Wizara ya Maliasili na
Utalii pamoja na halmashauri na ofisi yangu tukae pamoja ili kuweka
mkakati wa kuzuia matumizi ya kemikali hii,” alisema.
Wakati huohuo, kampuni zinazosafirisha au kutumia
kemikali nchini zimetakiwa kuwalinda kwa udi na uvumba wafanyakazi wao
ili zisiwaathiri.
Meneja wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Ofisi ya
Mkemia Mkuu wa Serikali iliyopo Mbeya, David Elias alisema hayo katika
hafla ya kuwakabidhi vyeti wakurugenzi 17 wa kampuni mbalimbali
zinazojihusisha na usambazaji na utumiaji wa kemikali.
Elias alisema pamoja na ofisi yake kuwa na
utaratibu wa kuwapima damu wafanyakazi wao, pia itaandaa mafunzo kwa
madereva wa magari yanayosafirisha kemikali. “Lazima tuwaelimishe hasa
maderava ambao wako kwenye hatari zaidi,” alisema Elias.CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment