Kwa mujibu wa taarifa kutoka mikoa kadhaa nchini, kuwa baadhi ya
shule zimelazimika kufungwa kutokana na kukosa chakula na kuwaacha
wanafunzi wenye mitihani ya Taifa wa kidato cha pili, nne na sita.
Mkoani Kagera, shule saba za sekondari zimefungwa kutokana na
ukosefu wa chakula na wanafunzi wa kidato cha kwanza, tatu na tano
wakirudishwa nyumbani kwa muda usiojulikana.
Hali hiyo inatokana na wazabuni wanaotoa huduma ya chakula kwa shule hizo kutolipwa fedha wanazodai.
Ofisa Elimu wa mkoa wa Kagera, Florian Kimolo, alisema wanafunzi
katika shule hizo wameongezewa muda wa kukaa nyumbani wakati huu ambao
serikali inatafuta ufumbuzi wa tatizo hilo.
Alizitaja baadhi ya shule hizo kuwa ni Rugambwa, Kahororo, Ihungo, Nyakato, Kimolo, Rukore, Kabanga na Muyenze za
Wilayani Ngara na kuwa tayari wamepeleka taarifa Ofisi ya Waziri
Mkuu (Tamisemi) kwa ajili ya kupatiwa fedha za chakula ili wanafunzi
warudi kuendelea na masomo.
“Kawaida binadamu yeyote anahitaji chakula na kinapokosekana siyo rahisi kuendelea kuishi na kuwa kumbakiza mwanafunzi
shuleni bila kumpa chakula kuna athari kubwa kiafya,” alibainisha na kuongeza.
“Kuwarudisha nyumbani kuna athari maana kunapunguza siku zao za masomo na wanaweza wasifundishwe baadhi ya mada.”
“Sifahamu lini wanafunzi hao watarejeshwa shuleni, lakini sisi kama
serikali tunafahamu madhara ya tatizo hilo, ndiyo maana tunafanya kila
jitihada ili warejee mapema iwezekanavyo” alisema.
Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba, Chacha Mwita, alithibitisha
kuwapo kwa tatizo hilo katika shule za sekondari za bweni na kuwa
jitihada zinaendelea ili wanafunzi warejee shuleni mapema iwezekanavyo.
Chacha alisema kuna madeni na kudai kuwa wazabuni hawajagoma kutoa
huduma na kuwa kuna kikao kimefanyika na mawasiliano yanaendelea
kufanyika ili waendelee kutoa chakula shuleni.
Hata hivyo, hakubainisha kiasi cha chakula kinachohitajika kwa shule zote na kuahidi kutoa taarifa kamili siku zijazo.
Mkoani Dodoma, shule za sekondari za bweni zimefungwa kwa muda usiojulikana kutokana na ukosefu wa chakula kwa wanafunzi.
Taarifa zilizolifikia NIPASHE zinaeleza kuwa moja ya shule hizo ni
Shule ya Sekondari Mpwapwa ambayo ilitakiwa kufunguliwa baada ya likizo
fupi ya sikukuu ya Pasaka lakini mpaka sasa haijulikani itafunguliwa
lini.
Mkuu wa shule hiyo, Nelson Mbilinyi, alisema wanafunzi walitakiwa
kufungua shule siku tatu zilizopita, lakini hadi sasa wameshindwa
kufungua shule kutokana na ukosefu wa chakula.
“Tulikuwa tufungue Aprili 8, mwaka huu, lakini hatujafungua hadi sasa chakula cha kuwalisha wanafunzi hakuna,” alisema.
Alisema bado hawajajua shule hiyo itafunguliwa lini, lakini kitu
ambacho anakijua ni kwamba leo kuna kikao na Afisa Elimu wa Mkoa.
Katika shule ya sekondari ya Wasichana Msalato iliyopo, Mkuu wa
Shule hiyo, Mwasi Chibuni, alisema shule hiyo haijafungwa isipokuwa hali
ya chakula si nzuri.
“Licha ya wanafunzi kuendelea na masomo, lakini hali ya chakula
siyo nzuri na shule haijafungwa tunaendelea tuone tutaishia
wapi,” alisema.
Alibainisha kuwa wataendelea kujisogeza hivyo hivyo na kama watashindwa, watalazimika kufunga shule.
Katika wilaya ya Kondoa, kuna taarifa kuwa hali ya chakula katika shule ya wasichana ya Kondoa ni mbaya na inaweza kufungwa.
Hata hivyo, Afisa Elimu sekondari wa wilaya hiyo, Lucy Gurtu,
alikanusha kuwa hakuna shule iliyofungwa kutokana na uhaba wa chakula.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Chiku Galawa, alipoulizwa kuhusu tatizo hilo, alijibu kuwa hana taarifa kwa sasa analifuatilia.
Mkoani Kilimanjaro, Serikali imesema itamchukulia hatua kali za
kisheria, ikiwa ni pamoja na kumsimamisha kazi, Mkuu yeyote wa shule ya
sekondari atakayebainika kushindwa kufungua shule kuanzia leo kwa
kisingizio kwamba shule yake haina chakula.
Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro (RAS), Alfred Shayo,
aliiambia NIPASHE jana kwa njia ya simu kwamba, tayari wamepokea fedha
kutoka Hazina, kwa ajili ya kuzihudumia shule za serikali.
“Kama kuna mkuu wa shule ambaye hatafungua shule katika muda uliopangwa, atachukuliwa hatua za kisheria kwa sababu Hazina
iliyopo chini ya Wizara ya Fedha, imekwishaleta hizo fedha za
chakula, ila kama zimechelewa kuwafikia wakuu wa shule, Ofisi ya Mkuu wa
Mkoa haina taarifa hizo...Kwa maana hiyo shule zote zitafunguliwa leo
kama kawaida.
Alisema ofisi hiyo haina taarifa yeyote ya shule za serikali mkoani
hapa kubadili ratiba ya masomo baada ya kumalizika kwa mapumziko ya
Pasaka kutokana na uhaba wa chakula.
Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama, alisema anachofahamu ni
wazabuni wengi kutolipwa fedha zao na kwamba hana takwimu za kiasi
wanachodai na shule zenye uhaba.
Shule nyingine zilizofungwani shule ya wavulana na wasichana Tabora
za mkoani Tabora, shule ya wavulana Nsumba mkoani Mwanza, shule ya
wasichana Masasi, Ndanda za mkoani Mtwara na shule ya sekondari ya
wavulana ya Songea, mkoani Ruvuma.
Mmoja wa wanafunzi wa shule ya sekondari Ndanda ambaye hakutaja
kutajwa jina lake, alisema wametakiwa kurudi nyumbani mwishoni mwa wiki
kwa kuwa hakuna chakula.
Shule ya wasichana ya Tabora, mmoja wa wanafunzi alithibitisha
kurudishwa nyumbani kwa wanafunzi wasio na mitihani ya Taifa mwaka huu,
tangu Machi 24, mwaka huu, kutokana na uhaba wa chakula.CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment