Wakati wimbi la ajali likiendelea kutikisa nchi, watu 220
wamefariki dunia kwa ajali za bodaboda nchini kuanzia Januari hadi Machi
mwaka huu, Kamanda wa Usalama barabarani, Mohamed Mpinga amesema.
Kamanda Mpinga alisema hayo jana mjini Kibaha
alipokuwa akifunga mafunzo kwa ajili ya madereva 1,000 wa bodaboda
mkoani Pwani, yaliyofadhiliwa na Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Moto
(AAT) kwa kushirikiana na asasi ya Fia ya nchini Uingereza.
Kwa mujibu wa kamanda Mpinga, vifo hivyo
vimetokana na ajali 668 zilizotokea nchi nzima katika kipindi hicho cha
miezi mitatu na ambazo zimesababisha majeruhi 618.
“Takwimu zinaonyesha kuwa mafunzo hayo ya madereva
wa bodaboda, yamefanikisha kupunguza idadi ya ajali kutoka 1,449
zilizotokea kati ya Januari na Machi mwaka 2014, hadi ajali 668 kati ya
Januari na Machi mwaka huu 2015,” alisema Kamanda Mpinga.
Katika kipindi hicho pia kumekuwa na punguzo
katika idadi ya majeruhi wanaotokana na ajali za bodaboda kutoka
majeruhi 1,304 mwaka jana 2014 hadi majeruhi 618 mwaka huu.”
Sababu ya vifo
Kamanda Mpinga alibainisha kuwa pamoja na idadi ya
ajali na majeruhi kupungua, vifo vimeongezeka na hili limetokana na
madereva wa bodaboda kutofuata sheria, kanuni na taratibu.
“Ukiangalia vifo vingi vilitokana na madereva
kutofuata sheria, kanuni na taratibu na hasa kutovaa kofia ngumu. Sasa
unaweza kuona kuwa bado tuna kazi nzito ya kuhakikisha vifo navyo
vinapungua.
Kamanda Mpinga aliwataka madereva waliomaliza
mafunzo ya awamu hiyo ya tano, kutumia vema elimu waliopata ili
kushiriki katika jitihada za Serikali na wadau wengine kukomesha tatizo
la ajali za barabarani.
Awali akimkaribisha kamanda Mpinga, Rais wa AAT
Nizar Jivani alisema mafunzo ya madereva hao 1,000 wa Mkoa wa Pwani, ni
mwendelezo wa mafunzo ya muda mrefu yaliyoanzia katika mkoa wa Dar es
Salaam, ambako madereva 4,000 walihitimu.
Aliwataka madereva hao kuwa mabalozi katika vita
dhidi ya ajali za barabarani ili kufikia lengo la kampuni hiyo kupunguza
ajali kwa asilimia 50.
Mwakilishi wa Fia , Monalisa Adhikari, alisema
taasisi hiyo ya Uingereza, itaendelea kutoa ufadhili wa mafunzo hayo
kadiri mahitaji yanavyoongezeka.CHANZO; MWANANCHI
No comments:
Post a Comment