Friday, 10 April 2015

JK: Utapiamlo tishio nchini.

Zaidi ya watoto milioni 2.7 nchini bado wanakabiliwa na tatizo la utapiamlo kutokana na lishe duni na iwapo hatua  hazitachukuliwa mapema kudhibiti hilo, watoto zaidi ya 500,000 watapoteza maisha ifikapo mwaka 2025.
 
Hayo yalibainishwa na Rais Jakaya Kikwete, wakati akifungua mkutano wa siku tatu wa dunia kuhusu masuala ya lishe duniani, jana jijini Dar es Salaam.
 
Kwa mujibu wa Rais Kikwete, serikali imekuwa na mikakati mbalimbali ya kukabiliana na utapiamlo nchini ukiwamo wa 2011/12   hadi 2015/2016 ambao umesaidia kupunguza idadi ya watoto wenye utapiamlo kutoka asilimia 42 mwaka 2010 hadi asilimia 34.7 mwaka uliopita.
 
Mikakati hiyo pamoja na mambo mengine, inalenga kuweka viini lishe kwenye vyakula na kwamba tangu kuzinduliwa kwake, takribani watu milioni 20 wamefikiwa na mazao ambayo tayari yamewekewa viini lishe.
 
Hata hivyo, alisema bado nchi ipo katika safari ndefu katika kufikia malengo ya milenia ya mkutano wa afya wa dunia na yale ya Tanzania ya mwaka 2025.
 
Rais Kikwete alisema wasiwasi  wa kutofikiwa kwa malengo hayo ya kidunia na yale ya kitaifa, unatokana na taifa kuwa na idadi kubwa ya watoto wenye tatizo la utapiamlo ambao kwa sasa ni takriban milioni 2.7.
 
Alisema, asilimia 58 ya watoto hao, wanatoka katika mikoa 10 nchini ambayo inakabiliwa na tatizo kubwa la lishe.
 
 Rais Kikwete alisema ushirikiano wa kutosha  kati ya serikali na wadau wengine zikiwamo sekta binafsi katika kukabiliana na suala hilo, vinginevyo, watoto takriban 580, 687 nchini wapo hatarini kupoteza maisha ifikapo mwaka 2025.
 
“Bado kuna njia ndefu kwa Tanzania ili iweze kufikia malengo ya milenia ya mkutano wa afya wa dunia ya mwaka 2020 na ya Tanzania ya mwaka 2025  ya kuboresha hali ya lishe,” alisema Rais Kikwete na kuongeza:
 
“Inakadiriwa kuwa, kuna zaidi ya watoto milioni 2.7 chini ya miaka mitano, bado wana udumavu ‘chronic malbutrition’.  Tafiti zinaonyesha kwamba, idadi ya watoto watakaofariki dunia kutokana na udumavu itafikia 580, 687 na kusababisha upotevu wa uzalishaji wa kiuchumi wa kiasi cha Dola milioni 20, 376CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment