Friday, 10 April 2015

Hatua za makusudi zichukuliwe kupambana na ugonjwa wa ini.

Katika toleo letu la gazeti hili la Aprili 7, mwaka huu kwenye ukurasa wa 10, tuliandika habari yenye kichwa cha habari `Ugonjwa wa homa ya ini wavamia Kigoma'.
 
Kwenye habari hiyo ilielezwa kuwa watu 1,393 wa kijiji cha Kasumo kata ya Kajana Wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma, wameugua ugonjwa unaoshukiwa kuwa ni wa homa ya ini.
 
Habari hiyo ilimkariri Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Shija Ganai, alipokuwa akizungumza na gazeti hili ofisini kwake  ambapo alisema mkoa huo ulipata taarifa ya kuwapo kwa mlipuko wa ugonjwa unaohisiwa kuwa ni wa homa ya ini kutoka kwa Mganga Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe Machi 8, mwaka huu.
 
Ganai alisema hadi kufikia Machi 3, mwaka huu, kulikuwa na taarifa za kuwapo kwa wagonjwa 1,393 kutoka katika kijiji cha Kasumo.
 
Alifafanua kuwa kati ya wagonjwa hao, 134 ni wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Misheni ya Mt. Rufino na Rinaldo na wengine 1,259 ni wananchi wa kijiji hicho. Ganai alisema watu hao walianza kuonyesha dalili za kuumwa kichwa, mwili kukosa nguvu, viungo vya mwili na tumbo kuuma huku baadhi yao wakitapika na kuharisha.
 
Kwa mujibu wa Ganai, wagonjwa wa awali walianza kupata dalili za ugonjwa huo Februari 28, mwaka huu. Aidha, alisema sampuli za wagonjwa zilichukuliwa na kupimwa katika maabara ya Hospitali ya Mkoa Maweni ambapo kati ya  sampuli 1,102 zilizopimwa, 255 zilionyesha kuwa wanaugua malaria.
 
Vile vile, alisema sampuli 17 zilipelekwa maabara ya Mkoa kutoka Zahanati ya kijiji cha Kasumo kwa ajili ya kupimwa ambapo kati ya hizo, tatu zilionyesha malaria na moja homa ya ini.
 
Aidha, alisema sampuli nyingine 17 zilipelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali jijini Dar es Salaam Machi 5, mwaka huu kwa uchunguzi zaidi na bado wanasubiri majibu. Alisema Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imewaelekeza wapeleke sampuli nyingine 60 kwa Mkemia Mkuu wa Serikali na juhudi ya kuzisafirisha zinafanyika.
 
Ganai alisema mlipuko wa ugonjwa huo unaonekana kufanana na ule uliotokea Septemba, 2013 katika kijiji cha Bukuba Wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma ambapo takriban watu 1,200 waliugua.
 
Wataalam wanaeleza kwamba kwa kawaida watu wengi hawaonyeshi dalili zozote za ugonjwa huo, jambo ambalo ni rahisi kuishi na virusi vya maradhi hayo na hivyo kusababisha maambukizi kwa wengine bila kugundulika. 
 
Hata hivyo, inaelezwa kuwa watu wengine husumbuliwa na homa kali na dalili ambazo hudumu kwa wiki kadhaa ambazo ni uchovu, kichefuchefu, mwili kuwa dhaifu, homa kali, kupoteza hamu ya kula, kupungua uzito, maumivu makali ya tumbo upande wa ini, macho na ngozi kuwa vya njano na mkojo kuwa mweusi. Kwa wagonjwa wengine, watalaam wanasema virusi vya ugonjwa wa ini hukua na kusababisha ini kuharibika ama saratani ya ini.
 
Na kwa bahati mbaya ugonjwa huu hauna tiba na ukifikia kiwango cha ini kuharibika au kupata saratani ya ini, hakuna jinsi ni kifo tu.
 
Ugonjwa wa ini huambukizwa kama ilivyo kwa Ukimwi kwa maana kwa njia ya kujamiiana, mate, jasho na mwingiliano wowote ule wa damu. Tafiti za kitaalam zinaonyesha kuwa virusi vya ugonjwa wa ini ni vya hatari kuliko hata vya Ukimwi. 
 
Kwa mujibu wa watalaam, hii inatokana na ukweli kwamba virusi vya maradhi ya ini vinaweza pia kuishi nje ya mwili wa binadamu, yaani nje ya mfumo wa damu kwa siku saba tofauti na virusi vya Ukimwi ambavyo huishi kwenye mfumo wa damu peke yake.
 
Ni kwa msingi huo ndipo tunapoona umuhimu wa kuchukuliwa kwa hatua za makusudi kuudhibiti ugonjwa huu hatari kuliko hata Ukimwi.
 
Inapaswa mamlaka zinazohusika zichukue hatua za haraka kuhakikisha kwamba ugonjwa huu hausambai kwa kasi na kuenea katika mikoa mingine.
 
Hatua zinazopaswa kuchukuliwa sasa ni pamoja na kutoa elimu kwa wananchi wafahamu dalili zake na jinsi unavyoambukiza.
 
Tunatoa tahadhari hiyo mapema ili isije ikatokea kama ilivyokuwa kwa ugonjwa wa Bonde la Ufa ulivyosambaa kwa kasi baada ya kuibuka hapa nchini miaka michache iliyopita.
 
Ugonjwa wa Bonde la Ufa ulianza kujitokeza katika mikoa ya wafugaji ya Arusha na Manyara, lakini katika kipindi kifupi, ulisambaa katika mikoa mingine na kusababisha vifo kwa mamia ya watu.
 
Kama walivyosema wahenga kwamba usipoziba ufa, utajenga ukuta, basi ni vema nasi tukaanza mapema kuudhibiti ugonjwa huu ili kuhakikisha kwamba hausambai kwa kasi katika mikoa mingine.CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment