.jpg)
Ajali ya Tanga ilihusisha mabasi ya Ngorika na Ratco ambayo
yaligongana uso kwa uso baada ya gari dogo aina ya Passo lililokuwa
likiendeshwa na Mbunge wa zamani wa Jimbo la Korogwe Vijijini, Mussa
Lupatu, kugonga ubavuni mwa basi la Ratco.
Miongoni mwa waliofariki dunia katika ajali ya Tanga, ni Lupatu na
mwanawe ambaye jina lake halijafahamika na wote walikuwa kwenye gari
aina ya Passo.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Juma Ndaki, alithibitisha
kutokea kwa ajali hiyo na kueleza kuwa ilitokea jana saa 5:30 asubuhi
katika kijiji cha Mbwewe, kata ya Mkata, Wilaya ya Handeni.
Alisema chanzo cha ajali hiyo ni gari dogo aina ya Toyota Passo
lenye namba T 628 PXC ikitokea uelekeo wa Mkoa wa Pwani kutaka kulipita
basi la Ngorika na kusababisha mabasi ya Ratco na Ngorika kugongana uso
kwa uso.
Kamanda Ndaki alisema katika ajali hiyo, dereva wa basi la kampuni
ya Ratco lenye namba T 665 CBR aina ya Yutong likitokea uelekeo wa Tanga
kuelekea Dar, alikatika miguu yote.
Alisema dereva wa basi kampuni ya Ngorika lenye namba T 770 BKW
lililokuwa likitokea Dar es Salaam kwenda Arusha, alifariki dunia papo
hapo.
Kamanda Ndaki alisema kati ya waliofariki dunia ni watoto watatu na
watu wazima saba wanawake wakiwa ni watano na wanaume wawili na
hawajatambuliwa majina yao.
Alisema baadhi ya waliopata majeraha makubwa walipelekwa katika
Hospitali ya Wilaya ya Handeni na wenye majeraha madogo wanatibiwa
katika Kituo cha Afya Mkata.
Alisema miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Korogwe ya Magunga.
Kamanda Ndaki alifafanua kuwa majeruhi 24 ni wa basi la Ngorika na
11 wa basi la Ratco na wanaendelea na matibabu katika Hospitali ya
Wilaya ya Handeni.
DAKTARI MKATA AZUNGUMZA
Daktari wa zamu katika Kituo cha Afya cha Mkata, ambaye hakutaka
kutajwa jina lake gazetini kwa kuwa siyo msemaji, aliliambia NIPASHE
katika eneo la tukio kuwa alipokea majeruhi 17, baadhi wakiwa katika
hali mbaya na kuhitaji kupata uangalizi wa karibu.
Alisema hospitali hiyo haina vifaa vya kisasa kulingana na mahitaji
ya majeruhi hao na dawa, hivyo kulazimika kuwapa rufaa ya kwenda
Hospitali ya Wilaya ya Handeni.
‘Nilipokea majeruhi wa ajali hiyo majira ya saa saba mchana, wengi
wakiwa katika hali mbaya, wameumia ndani kwa ndani na wengine kupasuka
vichwa, kuvunjika mbavu, mikono, miguu, mgongo, dereva mmoja amevunjika
miguu yote miwili huku kipande cha mguu mmoja hakikupatikana,”
alifafanua na kuongeza:
“Kutokana na kituo hiki kutokuwa na uwezo wa kuwahudumia, tumeomba msaada wa gari la wagonjwa la wilaya ili tuokoe maisha yao.”
Alifafanua kuwa majeruhi saba ni wanaume na wanawake watano ambao walitakiwa kupata uangalizi wa karibu.
MASHUHUDA WA AJALI WANENA
Mmoja wa mashuhuda wa ajali hiyo, Vai Simba Makame, ambaye
alishiriki kuchomoa miili ya majeruhi ndani ya magari hayo, alisema
aliona magari matatu yote yakiwa katika mwendo kasi katika eneo lenye
kona gari dogo aina ya Passo liligongwa na basi la Ngorika na baadaye
basi ya Ratco likigongana na Ngorika.
Alisema wakati wa uokoaji, mtoto mmoja ambaye alikuwa anavuka
barabara aligongwa na pikipiki na hali yake ni mbaya na kwamba
alikimbizwa hopitali ya wilaya.
Makame alisema alishuhudia miili ya marehemu ikipakizwa katika magari ya watu binafsi na kupelekwa hospitali kuhifadhiwa.CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment