Friday, 27 March 2015

KCMC-KCRI yatumia teknolojia mpya kutambua vimelea vipya

Tangu kuanzishwa kwake mwaka 2009, Taasisi ya Utafiti ya Kilimanjaro (KCRI) ya Shirika la Msamaria Mwema (GSF), iliyopo KCMC, imekuwa ikijenga uwezo wake wa kufanya tafiti ambazo ni kipaumbele kwa taifa.

Imeweza kusomesha wataalamu wake sehemu mbalimbali duniani kama vile Marekani, Uingereza, Uholanzi na Denmark.
Imeweza pia kuongeza miundombinu ya kufanyia tafiti hizo, ili kupata vielelezo sahihi vya kufahamu zaidi magonjwa pamoja na matibabu.
Kuanzia mwaka 2013, KCRI ikishirikiana na washirika wake kutoka Denmark (DTU) ilianza kujijengea uwezo wa utambuzi wa magonjwa kwa kutumia teknolojia mpya ya vinasaba ambayo inajulikana kama Whole Genome Sequencing (WGS).
Ili kufanikisha kasi ya utambuaji wa magonjwa, KCRI ilifunga mashine kadhaa zenye uwezo na teknolojia za kisasa.
KCRI inatumia mashine ya miseq ambayo ni ya kwanza kuletwa na kuanza kufanya kazi hapa Tanzania. Pia ni mojawapo ya mashine chache sana ambazo zipo Afrika.
WGS ni njia bora zaidi kuliko njia nyingine katika uchunguzi na utafiti utumiao vinasaba (DNA) kwa ajili ya utambuzi wa vimelea vinavyosababisha magonjwa.
Katika nchi zilizoendelea, hutumia mashine za namna hiyo katika huduma za afya, utafiti, ufuatiliaji na udhibiti wa magonjwa ya milipuko, kama vile kipindupindu na kifua kikuu.
Uchunguzi wa kutumia WGS unawezesha kusoma mtiririko mzima wa vinasaba vya kimelea chote.
Mpangilio wa vinasaba ni mtiririko wa taarifa nyeti sana zinazotumiwa na kimelea kuishi ndani ya mwili wa binadamu.
Mojawapo ya changamoto zinazoikabili sekta ya afya ni ongezeko kubwa la vimelea vyenye usugu dhidi ya dawa zitumikazo.
Pamoja na adha za kuchelewa kupona au dawa kushindwa kufanya kazi, usugu wa vimelea huleta mzigo mkubwa hasa kiuchumi.CHANZO: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment