Ni katika Kijiji cha Nyakabale kilichopo mjini Geita. Kijijini
hapo kuna nyumba nyingi zilizojengwa, unazoweza kuzifananisha na makambi
ya wakimbizi.
Wakazi wa eneo hilo wanaonekana wakichapa kazi,
huku magari yakipishana na pikipiki zilizobeba viroba vya mawe zikipita,
nyingine zikiwa zimebeba abiria wanne au zaidi mtindo maarufu wa
‘mshikaki’.
Hakika watu wa kijiji hiki hawakuwa wavivu kwani kila mtu alijishughulisha, si watoto, vijana, wanaume na wanawake.
Kwa juhudi wanazoonyesha, kama watu wote nchini
wangekuwa wakifanya kazi kama wanakijiji hawa, bila shaka Taifa
lingekuwa mbali kimaendeleo.
Walionekana wakibeba mawe, wengine wakianika udongo. Wengine wakiponda mawe, wengine wakifua dhahabu kwenye makarai na magunia.
“Lete mawe wewe acha kuzubaa, hali ya hewa
inabadilika, mvua muda wowote itanyesha,” alisikika kijana mmoja
akimwaambia mwenzake.
Pia makundi ya vijana yalikuwa yamebeba nyundo, sururu, wengine wakipanda, wengine wakishuka kutoka milimani.
“Oya, wahi mida ya kunywa chai,” alisikika mmoja wa vijana akihimiza wenzake saa nne asubuhi.
Hakika kijiji hiki kimechangamka, achilia mbali pilika nilizoziona, pia nilisikia kelele za mashine zikisaga mawe.
Zilikuwa ni kelele ya aina yake, zilizochangiwa na
muziki uliokuwa ukitokea kwenye baa, hata kusikilizana ilikuwa shida
kwangu, ingawa wenyeji walionekana kuzoea hali hiyo.
Ilikuwa ni kazi mtindo mmoja, starehe mtindo mmoja
kwani baadhi walikuwa kazini na wengine walionekana wakinywa pombe
asubuhi na mapema.
“Wewe mama ongeza bia moja, hapa ni starehe na
kazi mtindo mmoja ...leta tukushikie mtoto huyo. Mtakujaje na watoto
kazini?” kijana wa umri wa unaofikia miaka 18 alimhoji binti wa umri
wake aliyekuwa akiwahudumia.CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment