Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Rashid amesisitiaza
tamko la kupiga marufuku uvutaji wa sigara katika maeneo ya umma ili
kuilinda jamii kutokana na madhara yatokanayo na moshi wa sigara.
Tamko la Waziri limekuja ikiwa ni siku moja tu
baada ya maadhimisho ya Siku ya Kifua Kikuu Duniani, moja ya magonjwa
yanayosababishwa na uvutaji wa tumbaku.
Agizo hilo limezingatia Sheria ya Usimamizi wa
Bidhaa za Tumbaku, Sura ya 121 TL, ya mwaka 2003, Kipengele cha 12(1)
ambacho kinakataza matumizi ya bidhaa hiyo katika maeneo ya umma.
“Agizo hili linawataka wananchi wanaotumia bidhaa
za tumbaku, kupunguza au kuacha kabisa, pia linaijumuisha jamii yote
kujua madhara ya matumizi ya tumbaku na umuhimu wa kuzuia uvutaji katika
maeneo ya umma,” alisema Waziri katika tamko lake.
Uvutaji sigara ulianza kupigwa marufuku kwa mara
ya kwanza mwaka 1575 na Kanisa la Katoliki lakini katika karne ya 20
harakati dhidi ya uvutaji sigara zilipamba moto kwa sababu za kiafya.
Sababu kubwa ya kupiga marufuku ni ukweli kwamba
uvutaji sigara ni hiari wakati kuvuta pumzi ni lazima, hivyo mtu
anayetumia kilevi hicho hana budi kukaa mbali ili kuepusha uwezekano wa
kupata magonjwa kama ya moyo na saratani kwa wasiotumia na ambao kuvuta
pumzi ni lazima.
Msemaji wa wizara hiyo, Nsachris Mwamaja alisema
nia ya marufuku hiyo ni kuhakikisha wizara inatimiza kwa vitendo sheria
hiyo ya bidhaa za tumbaku kwa kupiga marufuku na kuchukua hatua za
kisheria. “Jamii itusaidie kutoa elimu katika hili, kuna suala la
kujenga maeneo maalum ya kuvuta sigara na elimu kwa wale wanaovuta,”
alisema.
Sheria ya usimamizi wa bidhaa za tumbaku ya mwaka
2003, inaeleza kuwa nia ni kuwalinda vijana wenye umri wa chini ya miaka
18 na wale wasiovuta wasishawishike kuvuta.
Kuwalinda wasiovuta wasipate madhara, kuifahamisha
jamii juu ya madhara ya tumbaku na madhara ya kuvuta moshi wa sigara
inayovutwa na mwingine na kuhakikisha jamii haina wavutaji sigara.
Maeneo ambayo yamepigwa marufuku kuvuta sigara
yametajwa katika tamko hilo kuwa ni katika ofisi zote za serikali na
taasisi zake, hospitali za umma, vyuo vikuu na shule za umma, vituo vya
usafiri wa anga, mabasi, bandari na treni, bustani, fukwe na katika
maeneo ya kupumzika ya umma.
Pia tamko hilo la wizara limekataza uvutaji wa sigara katika mikutano yote ya kiserikali.
“Wizara inawataka wale wote ambao wanataka kuacha
kabisa kuvuta sigara, wawatafute wataalamu wa afya ili wapate ushauri wa
kitaalamu,” alisema waziri katika tamko hilo.CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment