Aidha, atakayekutwa analima, kusambaza mbegu, kusafirisha,
kuzalisha au kuingiza mimea inayozalisha dawa za kulevya kama bangi,
mirungi na cocaine atatozwa faini isiyopungua Sh. milioni 20, kifungo
kisichozidi miaka 30 au vyote kwa pamoja.

Mbunge wa Mwibara (CCM), Kangi Lugola, alisema vita dhidi ya dawa
za kulevya inakuwa ngumu kutokana na tabia ya serikali kulinda
watuhumiwa hata pale ushahidi unapokuwa wazi.
Alisema ili kukomesha tabia hiyo, sheria hiyo inapaswa kutamka
kwamba watakaobainika kujihusisha na biashara hiyo adhabu ndogo iwe
kifungo cha maisha, kunyongwa hadi kufa au kupigwa risasi hadharani na
kwamba adhabu ya faini iondolewe.
“Bila hivyo, tutakuwa tunabadilisha chupa, lakini mvinyo ni ule
ule. Tatizo tulilonalo ni kulindana siyo vyombo vya usimamizi. Polisi
wakikamata
mfanyabiashara wa dawa hizi, simu za wakubwa zinapigwa wanawaachia,
kwa hiyo mimi sikubaliani na hili la kuanzisha mamlaka kama
hatutaondoa tatizo la kulindana,” alisema.
Alisema wafanyabishara wa dawa za kulevya wanajulikana kwa majina
hadi nyumba wanazoishi lakini hawachukuliwi hatua badala yake vyombo
vya dola vinahangaika kukamata wasafirishaji wadogo wadogo.
Aidha, alikiri kuwa na orodha ya majina na namba za nyumba
wanakoishi wafanyabiashara wa dawa za kulevya nchini, lakini hawezi
kuwataja bungeni
hapo kutokana na hali ya sasa kuonyesha kuwa mfumo mzima unawalinda wafanyabiashara hao.
Naye mbunge wa Mtera (CCM), Livingstone Lusinde, pamoja na kutaka
watakaokutwa na dawa za kulevya kunyongwa au kupigwa risasi
hadharani wiki mbili baada ya kuhukumiwa, pia aliitaka Serikali itafute
mbinu ya kuondoa dhana kuwa wafanyabiashara wakubwa wa dawa hizo
wanalindwa.
Mbunge wa Chambani (CUF), Yusuph Salim Hussein, aliungana na
wenzake na kutaka adhabu ya kifo cha kunyongwa au kupigwa risasi
hadharani kwa watakaojishughulisha na dawa za kulevya huku akisisitiza
adhabu hiyo ni stahiki kutokana na madhara makubwa ya dawa hizo kwa
jamii.
“Lakini pia naomba niulize inakuaje mtu anakutwa amemeza kete
tumboni za dawa za kulevya, anazitoa tumboni lakini hachukuliwi hatua
eti kwa
sababu ya uchunguzi, uchunguzi gani? Watu kama hawa wahukumiwe palepale,” alisisitiza.
Mbunge huyo alimtaja kijana mitano sasa, kwa kosa la kukutwa
akisafirisha dawa za kulevya, akisema tajiri aliyemtuma ambaye alimtaja
kwa jina moja la Dewji yuko nje na wala hajawahi kuhojiwa.
Mbunge wa Mbozi Magharibi (Chadema), David Silinde, alisema ni
wakati sasa Serikali ianze kufanyia kazi hukumu za kunyongwa
zinazotolewa na majaji kwa watuhumiwa wa mauaji ya watu wenye ulemavu wa
ngozi au kukutwa na kuuza dawa za kulevya ili kukomesha vitendo hivi.
“Sasa hivi kuna kesi za wauaji wa albino zimetolewa hukumu ya
kunyongwa, lakini mpaka leo hawa watu hawajanyongwa, kwa sababu Rais
hajasaini, sasa tunapendeza kunyongwa pia hawa dawa za kulevya, Rais
kabla hajaondoka madarakani, asaini wanyongwe,” alisisitiza.
Alisema serikali inapata kigugumizi cha kuwabana wafanyabiashara
wa kubwa wa biashara hiyo kwa kuwa ni matajiri wenye nguvu ya kufanya
jambo lolote kujilinda.
Awali, akiwasilisha muswada huo, Mhagama alisema katika kuiongezea
ukali sheria hiyo, adhabu za watu wote watakaoukutwa, kutumia,
kufadhili au kufanya dawa za kulevya zimeongezwa na kuwa kali zaidi.
Serikali inakusudia kuanzisha Chombo kinachojitegemea chenye
mamlaka ya kiutendaji ya kuchunguza, kupekua na kukamata watuhumiwa
tofauti na ilivyo Tume.
Nayo Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya Ukimwi, imeungana na
wabunge kwa kutaka adhabu ya faini iondolewe kwenye sheria hiyo
badala yake ibakie kifungo cha maisha au kunyongwa, pindi mtuhumiwa
atakapothibitika kuhusika na biashara hiyo.
Akiwasilisha maoni ya kamati hiyo, mbunge wa Viti Maalum (CCM),
Neema Himd, alisema wakulima wa mimea ya dawa za kulevya kama
bangi, kamati hiyo imependekeza kuwa watakaobainika waongezewe kifungo
na kusiwepo na faini.
Alisema Kamati pia imependekeza kuwa baadhi ya wadau wameeleza kuwa
hivi sasa wauza ‘unga’ wameanza kutengeneza wateja kwa kuweka dawa hizo
kwenye vyakula na vinywaji kwa wanafunzi wa shule za msingi na
sekondari, hivyo akapendekeza kuwa adhabu iwe kali ili kukomesha
uharamia huo.
Naye msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani katika Wizara hiyo, Rajab
Mohamed Mbarouk, alisema ili sheria hiyo iwe kali, lazima adhabu iwe
ni kifungo cha maisha au kunyongwa hadi kufa badala ya kuweka adhabu ya
faini au kifungo.
“Kambi rasmi inapendekeza kufuta masharti yote yanayotoa nafasi ya
kulipa faini kwa mtu atakayepatikana na biashara ya dawa za kulevya na
badala yake kuacha masharti ya kifungo pekee, hii itasaidia kukomesha
biashara hii haramu ambayo inaangamiza nguvu kazi ya Taifa,” alisema.CHANZO:NIPASHE
No comments:
Post a Comment